Oct 26, 2017 04:38 UTC
  • Boko Haram yaua wanajeshi sita wa Nigeria jimboni Yobe

Kwa akali wanajeshi sita wa Nigeria wameuwa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kushambulia kambi moja ya jeshi kaskazini mashariki mwa nchi.

Msemaji wa jeshi la Nigeria, Kanali Kayode Ogunsanya aliliambia shirika la habari la AFP jana Jumatano kuwa, wanamgambo hao walivamia kambi ya jeshi katika kijiji cha  Sasawa, yapata kilomita 45 kutoka mji wa Damaturu, makao makuu ya jimbo la Yobe na kuua askari kadhaa.

Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu idadi ya askari na wanachama wa Boko Haram waliouawa katika makabiliano ya risasi yaliyojiri baada ya kambi hiyo kuvamiwa.

Baadhi ya wanachama wa Boko Haram

Duru za habari zinasema kuwa, wanajeshi sita na wanachama kadhaa wa genge hilo la ukufurishaji wameuawa katika makabiliano hayo ya Jumanne usiku.

Kadhalika wapiganaji hao wa Boko Haram wameripotiwa kupora mali za umma na kuiba chakula wakati wa uvamizi huo katika kijiji cha Sasawa. 

Wiki iliyopita, wanajeshi watatu wa Nigeria waliuawa baada ya kushambuliwa na genge la kigaidi na la ukufurishaji la Boko Haram, katika eneo lililoko baina ya Damboa na Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno.

Tags