Oct 26, 2017 08:22 UTC
  • Mke wa kiongozi wa Boko Haram ya Nigeria ameuawa?

Jeshi la Nigeria linachunguza ripoti zinazoashiria kuwa mmoja wa wake wa kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, Abubakar Shekau ameuawa katika shambulizi la anga la hivi karibuni.

Olatokunbo Adesanya, Kamanda wa Kikosi cha Anga cha jeshi hilo amesema yumkini mke huyo wa Shekau aliyetambulika kama Fitdasi aliuawa pamoja na wanachama kadhaa wa Boko Haram katika shambulizi la anga la Oktoba 19, katika kijiji cha Durwawa, mjini Konduga, katika jimbo la Borno.

Shambulizi hilo la anga lilionekana kuwa la ulipizaji kisasi kwa kuzingatia kuwa, siku moja kabla ya hujuma hiyo ya jeshi la Nigeria, wanajeshi watatu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika waliuawa baada ya kushambuliwa na genge hilo la kigaidi na la ukufurishaji, katika eneo lililoko baina ya Damboa na Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno.

Mwanachama wa Boko Haram akiwa na mabinti waliowateka nyara

Fitdasi anaaminika kuwa mmoja wa wake wanne za Abubakar Shekau, huku mke mwingine akisemekana kuwa mjane wa muasisi wa genge hilo la ukufurishaji, Muhammad Yusuf ambaye alifia korokoroni nchini humo mwaka 2009.

Tangu kundi hilo lilipoanzisha mashambulizi yake mwaka 2009, limekwishaua zaidi ya watu elfu 20, na kupelekea zaidi ya watu milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Tags