Oct 28, 2017 02:39 UTC
  • Jeshi la Nigeria laangamiza wanachama kadhaa wa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limewaangamiza wanachama kadhaa wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni maalumu ya jeshi hilo kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Kanali Sani Usman, msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, kwa akali wanachama watatu wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia operesheni ya jeshi hilo katika msitu wa Sambisa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Kanali Sani Usman ameongeza kuwa, mwanzoni mwa wiki hii pia jeshi la Nigeria liliwaua wanachama 11 wa kundi la Boko Haram katika operesheni nyingine ya kijeshi katika maeneo hayo ya kaskazini mashariki mwa nchi ambayo ni ngome ya wanamgambo hao.

Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram

Tangu mwaka 2009, Nigeria imekuwa kishuhudia operesheni za kigaidi za kundi la kitakfiri la Boko Haram dhidi ya jeshi na raia hususan katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Genge la Boko Haram lilianzisha mashambulizi nchini Nigeria mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu za nchi za Magharibi. Zaidi ya raia 20 elfu wa Nigeria, Cameroon, Niger na Chad wameshapoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya genge hilo la kigaidi tangu wakati huo hadi hivi sasa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi.

Serikali ya Nigeria inayoongzwa na Rais Muhammadu Buhari imeendelea kukosolewa kutokana na kushindwa kulitokomeza kundi hilo la kigaidi ambalo limehatarisha usalama hata katika nchi jirani.

 

Tags