Ethiopia yatuma maelfu ya askari Somali kukabiliana na magaidi wa Al Shabab
Ethiopia imetuma maelfu ya askari katika nchi jirani ya Somalia kusaidia katika jitihada za kieneo za kupambana na kundi la magaidi wakufurishaji wa Al Shabab ambao wamekuwa wakitekeleza hujuma nchini humo na katika nchi jirani.
Wakaazi wa magharibi mwa Somalia wanasema Alhamisi walishuhudia maelfu ya wanajeshi wa Ethiopia wakivuka mpaka na kuingia nchini humo wakitumia magari ya deraya.
Wakuu wa Ethiopia wamethibitisha kutuma askari nchini Somalia na kusema hatua hiyo ni ya kawaida katika fremu ya kuzisaidia nchi za eneo kukabiliana na al-Shabab.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Meles Alem, amesema askari hao wameingia Somalia kwa mujibu wa majukumu ya nchi yake kama moja ya nchi zilizotuma wanajeshi katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM. Nchi zingine zinazochangia askari katika kikosi cha AMISOM ni pamoja na Burundi, Djibouti, Kenya na Uganda.

Askari hao Waethiopia wametumwa Somalia baada ya magaidi kutekeleza hujuma katika mji mkuu Mogadishu mnamo Oktoba 14 na kuua watu zaidi ya 300 katika shambulizi lililotajwa kuwa mbaya zaidi katika historia ya Somalia.
Baada ya hapo pia watu kadhaa wameuawa katika mashambnulizi ya kigaidi mjini Mogadishu ambapo kundi la kigaidi la Al Shabab lilidai kuhusika.
Rais Mohammad Abdulahi Mohammad wa Somalia ameapa kuimarisha mikakati ya kuwaangamiza magaidi wa al-Shabab.