Magaidi 10 waangamizwa katika Rasi ya Sinai nchini Misri
Jeshi la Misri limetangaza habari ya kuangamizwa magaidi 10 katika mkoa wa Sinai Kaskazini wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Mapema leo asubuhi, shirika la habari la IRNA limelinukuu jeshi la Misri likitangaza kuwa, askari wa nchi hiyo wamefanikiwa kuwaangamiza magaidi 10 katika operesheni maalumu iliyofanyika katika mji wa Sheikh Zuweid mkoani Sinai Kaskazini.
Vile vile jeshi la Misri limetangaza kuwa, askari wa nchi hiyo wamewatia mbaroni watu 22 wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na magaidi katika mji wa al Arish kwenye rasi hiyo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Mkoa wa Sinai Kaskazini wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mashambulizi ya magenge ya kigaidi likiwemo lile linalojiita Answar Bayt al Muqaddas ambalo mwezi Novemba 2014 lilitangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh na kujibadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.
Hadi hivi sasa genge hilo limefanya mashambulizi mengi dhidi ya wanajeshi, polisi na raia wa kawaida katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika hususan katika mkoa wa Sinai Kaskazini.