Wapinzani Misri: Mbinu ya serikali ya Cairo ya kuwakandamiza wapinzani imetoka Saudia
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa zamani na mwanaharakati wa kisiasa nchini Misri, amesema kuwa, serikali ya Cairo imeanzisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani kwa kutumia mbinu ya utawala wa Aal Saud nchini Saudi Arabia.
Masum Marzuq, Naibu wa zamani wa Waziri ya Mambo ya Nje ambaye pia ni mmoja wa wanaharakati wa kisiasa wa Misri amesema kuwa, kama vile ambavyo Mohammad bin Salman bin Abdulaziz Al Saud, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia anavyowatuhumu wapinzani wake kwa ufisadi na kisha kuwatia mbaroni, ndivyo serikali ya Misri pia inavyofanya kuwalenga shakhsia wa upinzani.
Ameongeza kwa kusema kuwa, serikali ya Cairo hutumia njia ya kuwadhalilisha na kuwatuhumu wapinzani kwa makosa ya jinai ili kwa njia hiyo kuwakandamiza wapinzani hao. Marzuq ameongeza kuwa, suala la kuwatuhumu wapinzani kwa tuhuma za ufisadi ni njia mpya iliyoenea sana ndani ya nchi za Kiarabu katika siku za hivi karibuni. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa zamani nchini Misri amesema kuwa, ili kujitenga mbali na ukosoaji mkubwa wa jamii ya kimataifa katika mchuano wa uchaguzi wa rais wa mwakani, hivi sasa serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi inafanya njama za kubuni tuhuma za jinai na ufisadi na kuwabebesha wapinzani wake.
Baada ya kuenea habari juu ya uwezekano wa Khalid Ali, wakili na mwanaharakati wa kisiasa nchini Misri kugombea katika uchaguzi wa rais mwakani, mwanaharakati huyto ameandamwa na kashfa nyingi za kimaadili kiasi kwamba, huenda asigombee tena katika kinyang'anyiro hicho.