Frankfurter Allgemeine: Utendaji mbaya wa serikali ya al Sisi unachochea ugaidi
Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linalochapishwa nchini Ujerumani limeshambulia vikali utendaji mbaya wa serikali ya Rais Abdul Fattah al Sisi nchini Misri na kusema inahusika kwa njia moja au nyingine katika kuchochea ugaidi.
Gazeti hilo limeashiria shambulizi la Ijumaa iliyopita katika Msikiti wa al Raudha katika jimbo la Sinai ambalo limeua Waislamu wasiopungua 305 waliokuwa katika Swala ya Ijumaa na kusema: Abdul Fattah al Sisi hajui chochote isipokuwa kutumia mabavu na ukandamizaji. Gazeti hilo limetahadharisha kuwa kiongozi wa sasa wa Misri anaielekeza nchi hiyo katika mustakbali wa kutisha.
Frankfurter Allgemeine limeandika katika toleo lake la leo kwamba, kuingia kwa vifaru katika mitaa ya Cairo na sherehe ya Wamisri wengi katika siku maarufu ya "Ghadhabu" hapo tarehe 28 January 2011 kuliwapa matumaini wakubwa Wamisri na kuwadhihirishia kuwa jeshi la nchi hiyo linawaunga mkono raia waliokuwa wakipambana na utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Husni Mubarak.
Gazeti hilo lenye idadi kubwa zaidi ya wasomaji nchini Ujerumani limeongeza kuwa: Matumaini yaliyojitokeza siku hiyo kwa Wamisri yamebakia kumbukumbu tu isiyokuwa na taathira yoyote na kwamba, mauaji ya Ijumaa iliyopita huko Sinai ni moja kati ya siku zilizowanyang'anya Wamisri matumaini ya mustakbali mwema.
Frankfurter Allgemeine limesisitiza kuwa jeshi la Misri lingali linatawala nchi kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Hosni Mubarak bali linafanya ukatili na kumwaga damu zaidi.
Gazeti hilo limeashia maelfu ya watu walioswekwa jela nchini Misri na mashaka makubwa yanayowasumbua raia wa kawaida wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa Abdul Fattah al Sisi amefeli katika mambo mengi.