Jeshi la Misri laangamiza magaidi 5 kaskazini mwa Cairo
Jeshi la Misri limefanikiwa kuangamiza wanachama watano wa magenge ya ukufurishaji baada ya kushambulia maficho yao kaskazini mwa mji mkuu, Cairo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema kuwa, magaidi hao walizidiwa nguvu baada ya kujiri makabiliano ya risasi baina yao na wanajeshi wa nchi hiyo hapo jana, katika kitongoji kilichopo kati ya miji ya Ramadan na Bilbeis, mkoani Sharqiya eneo la Nile Delta.
Ingawaje taarifa hiyo haijataja kundi linalohusishwa na wanachama hao wakufurishaji, lakini imeongeza kuwa, magaidi wengine sita wamekamatwa katika operesheni hiyo.
Jeshi la Misri lilishadidisha operesheni zake siku moja baada ya mamia ya watu kuuawa katika shambulizi la hivi karibuni la genge la kigaidi ambalo mpaka sasa halijajulikana, hujuma inayotajwa kuwa kubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waislamu zaidi ya 300 waliuawa na wengine zaidi ya 110 kujeruhiwa katika shambulizi la magaidi wakufurishaji dhidi ya msikiti mmoja wa Twariqa katika Peninsula ya Sinai nchini Misri.
Magaidi hao waliushambulia kwa bomu Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Al-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini wakati wa Sala ya Ijumaa, na kisha kuanza kuwamiminia risasi ovyo waumini waliokuwemo.