Wasenegal waunga mkono kupunguzwa muhula wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i3724-wasenegal_waunga_mkono_kupunguzwa_muhula_wa_rais
Idadi kubwa ya wananchi wa Senegal wameunga mkono azma ya kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi ili kupunguza muhula wa rais wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2016 10:40 UTC
  • Rais Sall wa Senegal
    Rais Sall wa Senegal

Idadi kubwa ya wananchi wa Senegal wameunga mkono azma ya kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi ili kupunguza muhula wa rais wa nchi hiyo.

Tume ya Uchaguzi nchini humo imesema asilimia 67 ya wananchi wamepiga kura ya ‘ndio’ ili kuunga mkono pendekezo hilo lililotolewa na Rais Macky Sall la kupunguza muhula wa rais kutoka miaka saba hadi mitano. Hata hivyo kura hiyo ya maoni ilishuhudia idadi ndogo ya wananchi.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, asilimia 38.3 ya wananchi waliotimiza masharti ya kupiga kura ndio walioshiriki katika zoezi hilo lililofanyika Jumapili iliyopita. Kadhalika marekebisho hayo ya katiba hayataruhusu mgombea wa kiti cha rais mwenye umri wa miaka zaidi ya 75, mbali na kuruhusu mgombea huru kuwania kiti cha rais, kinyume na ilivyokuwa huko nyuma. Marekebisho hayo ya katiba yanatazamiwa kuanza kutekelezwa baada ya uchaguzi ujao wa mwaka 2019.

Rais Macky Sall amekuwa akisisitiza kuwa, ili kuimarisha misingi ya demokrasia nchini humo, ameamua kupunguza muhula wake wa urais kwa miaka miwili. Kufanyiwa marekebisho katiba ya Senegal ni moja ya masuala aliyotumia Rais Sall wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Aghalabu ya nchi ambazo zilikuwa chini ya mkoloni Mfaransa zilirithi muhula wa miaka 7 wa rais kutoka Ufaransa, lakini chache kati yazo kama vile Kodivaa zimefanikiwa kupunguza muhula huo hadi miaka mitano.