Misri, Algeria, Tunisia zalaani uamuzi wa Trump kuhusu Quds
-
Sheikh al Azhar, Ahmed el-Tayeb
Nchi za Kiafrika za Misri, Tunisia na Algeria zimetoa taarifa tofauti za kulaani uamuzi wa rais wa Marekani, Donald Trump wa kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imesema katika taarifa yake kwamba uamuzi huo wa Trump ni ukanyagaji wa wazi wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Palestina na Baytul Muqaddas.
Kwa upande wake Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imetangaza kuwa, uamuzi huo wa Donald Trump umechukuliwa kwa makusudi ili kuchochea hasira za Waislamu.
Bunge la Misri nalo limelaani uamuzi huo wa serikali ya Marekani na kuonya kuhusiana na matokeo yake mabaya ya kiusalama.
Sheikh al Azhar naye amesema uamuzi huo wa Donald Trump ni kinyume cha sheria na kuwataka maulamaa wa Kiislamu kuitisha kikao cha dharura cha kuzungumzia njia za kuchukua kukabiliana na uadui huo mpya wa Donald Trump.
Uamuzi huo wa rais wa Marekani unaendelea kulaaniwa katika kila kona ya dunia huku kwenye baadhi ya maeneo kukiwa kunafanyika maandamano ya kulaani jaribio la Marekani la kuwapokonya Waislamu Kibla chao cha Kwanza yaani Masjidul Aqswa kupitia kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni.