Misri yawanyonga magaidi 15 walioua askari usalama Sinai
Misri imewanyonga watu 15 waliopatikana na hatua ya kufanya mashambulizi ya kigaidi yaliyoua askari usalama huko kaskazini mwa Peninsula ya Sinai.
Operesheni hiyo ya kunyonga wahalifu inatambuliwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kufanywa katika siku moja nchini Misri tangu Abdel Fattah al-Sisi alipochukua madaraka nchini humo mwaka 2014.
Watu hao wamenyongwa katika jela mbili za Borj al-Arab na Wadi al-Natroun zilizoko kaskazini mwa Misri mapema leo Jumanne.
Wengi kati ya watu hao walionyongwa walikamatwa katika jimbo la Sinai na walikabiliwa na tuhuma za kujiunga na makundi ya waasi na kufanya mashambulizi na mauaji dhidi ya askari jeshi na maafisa wa polisi.
Wapiganaji wa makundi ya kigaidi na kiwahabi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.
Shambulizi la hivi karibuni zaidi la matakfiri hao ni lile lililofanyika mwezi uliopita katika Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini. Zaidi ya Waislamu 300 waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala waliuawa katika shambulizi hilo.