Jan 02, 2018 15:00 UTC
  • Kiongozi wa Boko Haram aibuka, adai wamehusika katika mashambulizi

Kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, Abubakar Shekau ametoa kanda mpya ya video na kudai kuwa kundi hilo ndilo lililohusika na wimbi la mashambulizi ya bomu katika sherehe za kufunga mwaka, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Katika video hiyo ya dakika 31 hivi iliyotolewa leo Jumanne, Abubakar Shekau amekanusha madai ya serikali kwamba genge hilo la kigaidi linaelekea kusambaratika.

Amesema: "Tupo katika afya njema, hakuna chochote kilichotupata. Vyombo vya usalama vinaeneza propaganda dhidi yetu, haviwezi kututisha wala kutufanya chochote. Ni sisi tuliotekeleza mashambulizi ya hivi karibuni katika maeneo ya Maiduguri, Gamboru na Damboa."

Shekau ametoa video hii katika hali ambayo, genge hilo la kitakfiri limeshadidisha hujuma zake katika siku za hivi karibuni, shambulizi la hivi karibuni likiwa ni lile la Disemba 25 siku ya Krismasi katika mji wa Maiduguri, ambapo watu 25 waliuawa. 

Wanachama wa Boko Haram

Mashambulizi ya Boko Haram yalianza mwaka 2009 nchini Nigeria kwa madai ya kupinga elimu zinazotoka nchi za Magharibi.

Mashambulio ya genge hilo yalipanua wigo wake mwaka 2015 na kuingia pia katika nchi jirani na Nigeria, za Niger, Cameroon na Chad na hadi sasa zaidi ya watu 20,000 wanaripotiwa kuuawa kufuatia mashambulio hayo ya kigaidi ya wanamgambo wa Boko Haram.

Tags