Amnesty International yataka kuachwa kukandamizwa waandamanaji Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38891-amnesty_international_yataka_kuachwa_kukandamizwa_waandamanaji_tunisia
Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limeitolea wito kwa serikali ya Tunisia kuacha kutumia mabavu na kuwakandamiza wananchi wanaoandamana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 13, 2018 00:14 UTC
  •  Amnesty International yataka kuachwa kukandamizwa waandamanaji Tunisia

Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limeitolea wito kwa serikali ya Tunisia kuacha kutumia mabavu na kuwakandamiza wananchi wanaoandamana.

Sambamba na kushtadi maandamano ya malalamiko huko Tunisia, Amnesty International jana Ijumaa ilitoa taarifa ikiwataka askari usalama wa nchi hiyo kuheshimu haki za raia na kuacha kutumia mabavu dhidi ya wananchi wanaondamana kwa amani. Shirika hilo limewataka askari usalama wa Tunisia kuwadhaminia wananchi usalama wao badala ya kutumia nguvu dhidi yao. 

Polisi wa Tunisia wakikabiliana na wafanya maandamano 

Shirika la Msamaha Duniani limesisitiza katika taarifa yake hiyo  kuwa viongozi wa serikali ya Tunisia walipasa kuwadhaminia usalama na ulinzi waandamanaji na vikosi vya usalama kujiepusha na matumizi ya nguvu. 

Baadhi ya makundi nchini Tunisia jana Ijumaa pia yalimiminika mitaani katika maandamano ya kuishinikiza serikali ili isitishe uamuzi wake wa hivi karibuni. Wananchi nchini Tunisia walianza kuandamana tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari kufuatia kupasishwa sheria mpya ambapo bei ya bidhaa na kodi imeongezeka. Serikali ya Tunis imeamua kutekeleza siasa za kubana matumizi kufuatia kupungua kwa kiasi kikubwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo na kuwepo nakisi ya bajeti. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza kuwa karibu watu 780 wametiwa mbaroni kuanzia Jumatatu iliyopita hadi sasa yalipoanza maandamano ya wananchi katika miji mbalimbali nchini  kulalamikia ongezeko la bei ya bidhaa na kodi.