Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali inavyoendelea nchini Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38907-umoja_wa_mataifa_watiwa_wasiwasi_na_hali_inavyoendelea_nchini_tunisia
Umoja wa Mataifa umesema umetiwa wasiwasi na idadi kubwa ya watu waliotiwa mbaroni nchini Tunisia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 13, 2018 04:17 UTC
  • Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali inavyoendelea nchini Tunisia

Umoja wa Mataifa umesema umetiwa wasiwasi na idadi kubwa ya watu waliotiwa mbaroni nchini Tunisia.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza wasiwasi wa umoja huo kuhusu idadi kubwa ya watu waliokamatwa nchini Tunisia walioandamana katika miji mbalimbali kulalamikia kupanda kupindukia bei za bidhaa nchini humo na kusema kuwa, sehemu kubwa ya waandamanaji hao wamechoshwa na siasa za kubana matumizi za serikali ya Tunis.

Maandamano ya wananchi nchini Tunisia

 

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, karibu watu 800 wametiwa nguvuni nchini Tunisia tangu Jumatatu iliyopita hadi hivi sasa.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, mtu mmoja ameuawa katika machafuko hayo ya hivi karibuni.

Malalamiko ya wananchi wa Tunisia yalianza mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, 2018 baada ya serikali ya Tunis kupasisha sheria ya kuongeza bei za bidhaa na kukata ruzuku.

Serikali ya Tunisia imekumbwa na nakisi kubwa ya bajeti kutokana na kuporomoka thamani ya sarafu ya nchi hiyo, hivyo imeamua kutekeleza siasa za kubana matumizi, siasa ambazo zimesababisha matatizo makubwa ya kimaisha kwa wananchi ambao wamemiminika mitaani kulalalamikia ugumu usiovumilika wa maisha.