Algeria: Genge la Daesh (ISIS) linapanga kufanya mashambulizi makali Afrika
Gazeti la al-Khabar la Algeria limeandika kuwa, kundi hatari la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) linapanga kufanya operesheni kubwa za kigaidi katika nchi za Kiafrika.
Gazeti hilo sambamba na kuelezea harakati za makundi ya kigaidi hususan Daesh barani humo, limeandika kwamba, hadi sasa kuna wanachama wengi wa ISIS wanaoendesha harakati zao nchini Libya, Nigeria na Mali, yakiwemo pia maeneo yanayopakana na Algeria, ambao kwa mujibu wa taarifa ya vyombo vya usalama, magaidi hao wa Kiwahabi wamepanga kufanya mashambulizi makali ya kigaidi barani humo. Gazeti la al-Akhbar limeongeza kwamba, hivi karibuni Naibu Waziri wa Ulinzi wa Algeria, Ahmed Gaid Salah alitoa amri kwa makamanda wote wa jeshi katika maeneo ya mpakani ya nchi hiyo kuchukua tahadhari juu ya harakati za makundi ya kigaidi.
Baada ya kuangamizwa genge la wakufurishaji la Daesh (ISIS) katika nchi za Iraq na Syria, sasa magenge yenye misimamo mikali ya kigaidi hususan Daesh yametangaza kuunda muungano mpya unaojulikana kwa jina la "Kundi la Daesh katika Jangwa la Sahara." Kingozi wa kundi la Daesh katika eneo la kaskazini mwa Afrika anaitwa Adnan Abu al Walid al Sahrawi ambaye ni muhusika mkuu wa mashambulizi ya kigaidi katika eneo la Sahel barani Afrika.