Kenya kuisaidia Somalia kuiumarisha mfumo wa sheria
Mwanasheria mkuu wa Kenya, Githu Muigai amesema, nchi yake itaisaidia Somalia kuimarisha mfumo wake wa sheria, ili kukabiliana vizuri zaidi na na changamoto za kijamii na kisiasa.
Muigai amesema hayo mjini Nairobi alipokutana na ujumbe wa Somalia uliokuwa ziarani Nairobi na kuongeza kuwa Kenya itaipa Somalia utaalamu wa kuisaidia kujenga upya mfumo wake wa sheria.
Vilevile ameongoza kuwa, karibuni hivi Kenya itaanza kutoa mafunzo kwa maofisa wa sheria wa Somalia ili kuongeza uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao kwa haki.
Manasheria mkuu wa Kenya amesema, Nairobi na Mogadishu zinalenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiufundi ili kutumia kwa pamoja vyanzo vya bahari za nchi hizo mbili jirani.
Waziri wa sheria wa Somalia Bw. Hassan Hussein Haji ameongoza ujumbe uliofanya ziara ya siku mbili nchini Kenya, kwa lengo la kujifunza uzoefu wa Kenya katika kuimarisha mfumo wa kisheria.
Haji amesema Somalia inaitazama Kenya kama mshirika mkubwa katika kuijenga nchi hiyo baada ya robo karne ya vita vya ndani.