Wanamgambo wenye silaha wafanya ubakaji mkubwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wanamgambo wenye silaha mwezi uliopita waliwashambulia, kuwateka nyara na kubaka kwa umati kundi kubwa la wanawake katika eneo moja lililotengwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hayo yameelezwa na Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).
Jumuiya hiyo imeeleza katika taarifa yake kuwa taasisi hiyo iliwapatia matibabu manusura kumi wa uhalifu huo uliofanywa tarehe 17 mwezi uliopita wa Februari karibu na kijiji cha Kiriwiri kinachopatikana kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Imeongeza kuwa, wanawake hao waliokumbwa na mkasa wa kubakwa walishindwa kutafuta matibabu hadi baada ya kupita wiki mbili wakihofia kukabiliwa na mashambulizi zaidi iwapo watajaribu kwenda hospitali.
Aidha wahanga wengine wengi wa ubakaji huo wameshindwa kujitokeza wakihofia kunyanyapaliwa na jamii baada ya kubakwa.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko baada ya waasi wa Muungano wa Seleka kumuondoa madarakani Rais wa zamani wa nchi hiyo Francois Bozize mwaka 2013. Tukio hilo lilifuatiwa na mauaji yaliyofanywa na wanamgambo wa Kikristo wa kundi la Anti Balaka.