Rais wa Mauritius ajiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41453-rais_wa_mauritius_ajiuzulu_kutokana_na_kashfa_ya_ufisadi
Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Jugnauth amesema kuwa rais wa nchi hiyo Ameenah Gurib-Fakim ameamua kujiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi inayomuandama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2018 04:21 UTC
  • Rais wa Mauritius ajiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi

Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Jugnauth amesema kuwa rais wa nchi hiyo Ameenah Gurib-Fakim ameamua kujiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi inayomuandama.

Jugnauth aliyasema hayo Alkhamis huko Port Louis, mji mkuu wa kisiwa hicho kilichoko katika bahari ya Hindi na kubainisha kuwa, sakata la ufisadi wa kifedha linalomsakama rais huyo limemsukuma ukutani na kuamua kuachia madaraka.

Amesema, na hapa tunanukuu, "Tumekubaliana na rais kuhusiana na yeye kujiuzulu." Awali ilitangazwa kwamba rais huyo angejiuzulu rasmi Jumatatu ijayo ya Machi 12, baada ya nchi hiyo kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wake.

Port Louis, mji mkuu wa kisiwa cha Mauritius

Ameenah Gurib-Fakim, ambaye ndiye rais mwanamke pekee kwa sasa barani Afrika, anatuhumiwa kuchota fedha kutoka kwenye akaunti ya Asasi Isiyokuwa ya Kiserikali ya Planet Earth Institute yenye makao yake London Uingereza, na kutumia fedha hizo katika masuala ya kibinafsi. Gurib-Fakim mwenye umri wa miaka 58 amekuwa rais wa kwanza mwanamke katika historia ya kisiwa hicho, tokea mwaka 2015.