Apr 01, 2016 04:22 UTC
  • Mripuko ndani ya msikiti waua watu wawili na kujeruhi 15 nchini Somalia

Watu wawili wameuawa na wengine 15 wamejeruhiwa wakati ulipotokea mripuko ndani ya msikiti katika mji wa Beledweyne mkoani Hiiraan katikati mwa Somalia hapo jana.

Hata hivyo wakaazi wa eneo hilo na Polisi wamesema kuna uwezekano mkubwa mripuko huo ulitokana na ajali na si shambulio la kigaidi.

Afisa wa Polisi aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Ibrahim amevieleza vyombo vya habari kuwa wanaamini kuwa gurunedi lililodondoshwa kwa bahati mbaya na watu waliokuwa wakisali msikitini humo ndilo lililosababisha mripuko huo.

Aidha Ahmed Nour, mmoja wa wazee wa mji wa Beledweyne naye pia amesema msikiti huo hakushambuliwa, bali lilikuwa ni tukio la ajali ya bahati mbaya. Ameongeza kuwa hawajawahi kushuhudia misikiti ikishambuliwa na kwamba kama tukio hilo lingekuwa limesababishwa kwa makusudi lingeweza kuua watu wengi kirahisi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo siku ya Jumatano watu sita, wakiwemo Waturuki wawili waliuawa katika shambulizi lililolenga basi dogo lililokuwa limebeba wafanyakazi wa hospitali moja inayosimamiwa na Uturuki katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Raia wengine 6 wa Uturuki na Mkenya mmoja walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kigaidi.../

Tags