Mar 23, 2018 07:22 UTC
  • Mzozo wa uongozi wapelekea msikiti kufungwa na kuzingirwa Uganda

Wanajeshi na maafisa wa polisi wameufunga na kuuzingira Msikiti wa Basajjabalaba katika Manispaa ya Bushenyi-Ishaka magharibi mwa Uganda kutokana na mzozo miongoni mwa Waislamu katika eneo hilo.

Ronald Rutaro, Kamanda wa Polisi katika wilaya ya Bushenyi amesema msikiti huo umefungwa tangu Jumapili iliyopita hadi sasa, baada ya kundi la watu kuushambulia msikiti huo kwa silaha wiki iliyopita.

Amesema, "Tulipokea taarifa kwamba kuna kundi la vijana wa Kiislamu liliuvamia msikiti huo kwa mapanga na mikuki na tulipotuma maafisa wetu tuliweza kugundua silaha hizo, na ndiposa tukaamua kuufunga ili kuzuia maafa."

Waislamu wa Uganda katika marasimu huko nyuma

Duru za habari zimefichua kuwa, kikundi cha Waislamu wa eneo hilo kimesema hakiridhishwi na uongozi wa Mubarak Kateinama, ambaye ni Kadhi wa wilaya ya Bushenyi na wanamtaka ajiuzulu mara moja.

Sheikh Shaban Ramadhan Mubajje, Mufti Mkuu wa Uganda ameingilia kati kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo, huku polisi ikisisitiza kuwa maafisa usalama wataendelea kuuzingira msikiti huo hadi mambo yatangamae.

 

Tags