Waziri Mkuu wa Tunisia: Nipo tayari kujiuzulu
Waziri Mkuu wa Tunisia ametangaza kuwa yupo tayari kujiuzulu wadhifa huo kwa masharti.
Youssef Chahed ametangaza leo kuwa yupo tayari kujiuzulu cheo cha Waziri Mkuu mkabala na kutosimamishwa mchakato wa mageuzi aliyoyaunga mkono nchini Tunisia.
Al Chahed ameongeza kuwa marekebisho ya kiuchumi hususan katika sekta ya taasisi za umma yanapasa kuanza kwa kasi na kwamba moja ya njia ya kuondoa nakisi ya bajeti iliyopo ni kukabidhiwa baadhi ya taasisi za serikali kwa sekta binafsi.
Youssef Chahed ambaye mwezi Agosti mwaka juzi aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tunisia, hivi sasa yuko chini ya mashinikizo makubwa ya wapinzani hususan jumuiya za wafanyakazi na anatuhumiwa kuwa amefeli katika siasa za uchumi. Baadh ya maeneo nchini Tunisia ikiwemo miji ya al Redeyef huko magharibi na Mdhila katikati mwa Tunisia katika wiki za karibuni iliathiriwa na migomo na maandamano ya kulalamikia matatizo ya kiuchumi na kijamii likiwemo tatizo la ukosefu wa ajira.
Gavana wa Benki Kuu ya Tunisia pia ametahadharisha juu ya mfumuko wa bei nchini humo.