Jeshi la Mali laua 'magaidi 14 wakitoroka jela'
Jeshi la Mali limesema kuwa limeua wapiganaji 14 wa genge moja la kigaidi walipojaribu kutoroka jela.
Taarifa ya Jeshi la Mali imesema kuwa, washukiwa hao wa ugaidi waliuawa jana Ijumaa wakijaribu kutoroka jela katika mji wa Dioura katikati ya nchi, siku moja baada ya kukamatwa kwa ajili ya kusailiwa.
Hata hivyo maafisa wawili wa serikali katika eneo hilo wamenukuliwa na shirika la habari la AFP wakitilia shaka jaribio hilo la kutoroka jela, na kusema raia 20 wameuawa au kukamatwa na wanajeshi katika mji wa Dioura.
Jumapili iliyopita, Jeshi la Ufaransa lilitangaza kuwa limeua wapiganaji 30 wa kundi moja la kigaidi nchini Mali kwa kushirikiana na wanajeshi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, karibu na mpaka wa Niger.
Nchi ya Mali inakumbwa na machafuko na mashambulizi ya kigaidi tangu mwaka 2012 wakati yalipotokea mapinduzi ya kijeshi na kuzuka uasi kaskazini mwa nchi hiyo, uliopelekea kutekwa eneo kubwa la nchi hiyo na waasi.
Askari wa Umoja wa Mataifa pamoja na wale wa mkoloni Ufaransa walitumwa nchini Mali katikati ya mwaka 2013, lakini pamoja na hayo wameshindwa kuzima uasi huo na harakati za kigaidi licha ya kukomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yametekwa.