Zarif awasili ziarani Windhoek, Namibia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Windhoek mji mkuu wa Namibia katika marhala ya mwisho ya ziara yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za Amerika ya Latini na Afrika.
Kabla ya kuelekea Namibia, Muhammad Javad Zarif alikuwa tayari amefanya ziara nchini Uruguay; hiyo ikiwa ni marhala yake ya tatu katika ziara yake hiyo ya kiduru. Akiwa nchini Uruguay, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Rais, Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje, Spika wa bunge na seneti na kushiriki pia katika mkutano wa kibiashara kati ya Iran na nchi hiyo.
Zarif pia alizizuru Brazil na Senegal kabla ya kuelekea Uruguay. Katika ziara hiyo,mbali na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi mbili hizo, kufanya mashauriano kuhusu kustaiwsha uhusiano wa pande mbili na kuchunguza matukio ya karibuni kieneo na kimataifa; Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile alipata fursa ya kushiriki katika vikao vya kiuchumi na kibishara kati ya pande mbili.
Safari hiyo ya kiduru ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika nchi kadhaa za Kiafrika na Amerika ya Latini ilianza Jumapili iliyopita. Katika ziara zake hizo, Muhammad Javad Zarif ameongozana na ujumbe wa kisiasa na kiuchumi unaowajumuisha wafanyabishara na wakurugenzi mbalimbali wa makampuni ya Kiirani.