Upinzani nchini Madagascar wakataa upatanishi wa UN
(last modified Tue, 08 May 2018 16:55:35 GMT )
May 08, 2018 16:55 UTC
  • Upinzani nchini Madagascar wakataa upatanishi wa UN

Upinzani nchini Madagascar umepinga upatanishi wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro unaoendelea kutokota katika kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa Afrika.

Hanitriniaina Razafimanantsoa, mbunge wa upinzani amewaambia wafuasi wao waliokuwa wanaamdana kwa siku ya 17 katika mji mkuu Antananarivo kuwa, "Huu ni mgogoro ambao utapatiwa ufumbuzi na Wamadagascar wenyewe, hatutaki upatanishi wa mjumbe wa UN aliyetumwa nchini."

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa, Abdoulaye Bathily, aliwasili nchini Madagascar Jumapili iliyopita kwa ajili ya kujaribu kuhuisha mazingira ya kufanyika mazungumzo kati ya maafisa wa serikali na wakuu wa upinzani kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Msimamo huo wa upinzani unatolewa katika hali ambayo, siku chache zilizopita Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo katika kile kilichoonekana ni kujaribu kushusha joto la kisiasa na kupunguza ghadhabu za waandamanaji, ilitangaza kufuta baadhi ya sheria mpya za uchaguzi zinazopingwa na wapinzani.

Maafisa wa polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Antananarivo

Tangu tarehe 21 Aprili, wapinzani wa Rais Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kubatilishwa sheria za uchaguzi zilizopasishwa hivi karibuni ambazo walizitaja kuwa na upendeleo, sanjari na kumtaka rais huyo kujiuzulu.

Marc Ravalomanana aliyewahi kuwa rais wa Madagascar anashirikiana na aliyemrithi kiti hicho, Andy Rajoelina, kupinga marekebisho na sheria hizo mpya za uchaguzi.