May 20, 2018 14:29 UTC
  • Chanjo ya Ebola kuanza kutolewa Kongo DR kesho Jumatatu

Wafanyakazi wa sekta ya afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wataanza kupewa chanjo ya Ebola kesho Jumatatu katika juhudi za kuzuia kuenea ugonjwa huo hatari.

Msemaji wa wizara ya afya ya nchi hiyo Jessica Ilunga amesema dozi 4,000 za Ebola ziliwasili jana Jumamosi katika mji wa Mbandaka ambao wiki iliyopita uliropoti kesi za kwanza za ugonjwa huo mjini humo baada ya kuripotiwa kuibuka nchini humo mapema mwezi huu.

Mripuko wa hivi karibuni wa Ebola ndio wa tisa tangu ugonjwa huo uripotiwe huko DRC muongo wa 70. Kuripotiwa kesi za Ebola katika mji wa bandarini wa Mbandaka katika Mto Kongo kumeibua wasiwasi kuwa yamkini kirusi hicho hatari kikafika katika mji mkuu Kinshasa ambao una idadi ya watu milioni 10.

Shirika la Afya Duniani limesema litatuma dozi 7,540 za chanjo ya Ebola nchini Kongo. Chanjo hiyo imetegenezwa na shirika la Merc na kuna tetesi kuwa shirika jingine la kutegeneza madawa la Johnson & Johnson nalo pia liko mbinoni kuzalisha chanjo ya Ebola.

Mazishi ya mtu aliyefariki kwa Ebola

Kwa mujibu wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, watu wasiopungua 18 wamefariki dunia nchini humo tangu kesi mpya za ugonjwa wa Ebola ziliporipotiwa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo tarehe tisa mwezi huu wa Mei tisa.

Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mripuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan kwenye nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mripuko wa Ebola uliotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani. 

Tags