May 23, 2018 14:35 UTC

Wagonjwa watatu walioambukizwa ugonjwa hatari wa Ebola wametoroka eneo la karantini walimokuwa katika hospitali moja huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mji wa Mbandaka huku madakatari wakiwa mbioni kuzuia ugonjwa huo hatari kuenea.

Mkuu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) mjini humo Henry Gray amesema wagonjwa wawili walitoroka Jumatatu na walipatikana wamefariki Jumanne huku mwingine aliyetoroka Jumamosi akipatikana siku hiyo hiyo na sasa anaendelea kupewa matibabu.

Amesema hospitali ambayo imeweka eneo la karantini si gereza na hivyo ni vigumu kuzuia watu kikamilifu kutoka au kuingia.

Ripoti hiyo imekuja wakati ambapo Shirika la Afya Duniani WHO limeonya kuwa mripuko wa Ebola nchini DRC umefika kiwango hatari. Mkuu wa  idara ya masuala ya dharura katika WHO Peter Salama amewaaambia mawaziri wa afya wa nchi mbali mbali duniani waliokutana Geneva kuwa kipindi cha wiki chache zijazo kitakuwa muhimu katika kubaini iwapo Ebola itaenea katika miji mingine huko DRC na iwapo kutakuwa na uwezo wa kudhibiti ugonjwa huo hatari au la.

Chanjo ya Ebola

Wafanyakazi wa afya wana hofu kubwa kuwa ugonjwa huo unaweza kuenea hadi katika mji mkuu Kinshasa wenye watu milioni 10, kutokana na kuwa, kitovu cha ugonjwa huo ni mji wa bandarini wa Mbandaka ambao uko katika mto Congo na ni kituo muhimu cha biashara. Ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza mapema mwezi huu na hadi sasa watu 27 wameshafariki dunia.

Jumatatu ya wiki hii wafanyakazi wa sekta ya afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameanza kupewa chanjo ya majaribio ya Ebola katika juhudi za kuzuia kuenea ugonjwa huo hatari.

Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mripuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan kwenye nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mripuko wa Ebola uliotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.

Wakati huo huo Serikali ya Congo Brazzaville imefunga mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama njia ya kujikinga na kuenea ugonjwa huo nchini humo.

Mwandishi wetu Mossi Mwasi ametuandalia ripoti maalumu kuhusu suala hilo...

 

Tags