May 28, 2018 03:51 UTC
  • Chanjo ya Ebola yaanza kutolewa vijijini Kongo DR

Wizara ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo Jumatatu inaaza kupeana chanjo ya ugonjwa hatari wa Ebola katika vijiji viwili vilivyoathiriwa na mlipuko wa sasa wa maradhi hayo.

Tayari utoaji wa chanjo hiyo unaendelea katika mji wa Mbandaka wenye watu milioni 1.2, ambao kesi nne za kwanza za ugonjwa huo zilithibitishwa.

Jessica Ilunga , Msemaji wa Wizara ya Afya nchini humo amesema kampeni ya chanjo hiyo itaanza leo Jumatatu katika vijiji vya Bikoro na Iboko.

Takwimu za wizara hiyo zinaonesha kuwa, katika kesi 10 za ugonjwa huo zilizothibitishwa kufikia sasa, 5 zimeripotiwa katika kijiji cha Bikoro, 2 Iboko na 3 katika maeneo ya Wangati mjini Mbandaka.

Maafisa wa afya wakipeana chanjo ya Ebola DRC

Shirika la Afya Duniani WHO limeonya kuwa mripuko wa Ebola nchini DRC umefikia kiwango hatari,  na yumkini Ebola itaenea katika miji mingine huko DRC na hata nchi jirani iwapo ugonjwa huo hatari hautadhibitiwa.

Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mripuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan kwenye nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mripuko wa Ebola uliotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.

 

Tags