Jun 17, 2018 15:15 UTC
  • Waislamu 31 waliokuwa wanasherehekea Idi wauliwa na Boko Haram nchini Nigeria

Watu wasiopungua 31 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika miripuko ya mabomu iliyotokea usiku wa kuamkia leo kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, katika mashambulizi hayo yanayoaminika kufanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram, magaidi hao waliilenga mikusanyiko wa Waislamu ambao walikuwa wanarejea majumbani mwao baada ya pirikapirika za sherehe za Idul-Fitr mwendo za saa tano kasorobo usiku, katika vitongoji vya Shuwari na Abachari mjini Damboa jimboni Borno.

Habari zaidi zinasema kuwa, baada ya magaidi waaliyokuwa wamejifunga mabomu kujiripua kwenye mikusanyiko hiyo ya watu, magaidi wenzao ambao walikuwa mbali kidogo na eneo la tukio walianza kuvurumisha maguruneti kwenye mikusanyiko hiyo ili kuongeza idadi ya wahanga.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Babakura Kolo, mmoja wa makamanda wa genge hilo la ukufurishaji akizungumza kutoka Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, umbali wa kilomita 88 kutoka mji wa tukio, amesema: "Hakuna anayehitaji kuambiwa kwamba hiyo ni kazi ya Boko Haram."

Tokea kundi la kigaidi la Boko Haram lianzishe uasi wake nchini Nigeria mwaka 2009, watu zaidi ya 20 elfu wameuawa, huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na ugaidi wa kundi hilo.

Kwa sasa wigo wa harakati na mashambulio ya Boko Haram umepanuka hadi katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.

Tags