Aug 04, 2018 08:12 UTC
  • WHO yatangaza azma ya kukabiliana na Ebola DRC

Shirika la Afya Duniani WHO, limesema litafanya kila liwezalo kudhibiti kuenea kwa mlipuko wa Ebola ambao umethibitishwa huko jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Dkt. Peter Salama ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa WHO anayehusika na masuala ya dharura amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi Ijumaa kuwa tayari wameanza kuweka  mikakati madhubuti ya kudhibiti mlipuko huo wa 10 nchini DRC wakati huu ambapo kuna ripoti za vifo ambavyo havijathibitishiwa kuwa vimetokana na Ebola.

Amesema, WHO imefanya tathmini  ya tishio la maambukizi na kubaini kuwa hatari ni kubwa na ni ya juu sana kwa ngazi za kitaifa, na pia kwa ngazi ya kikanda, na ni ya chini kwa ngazi ya kimataifa.

Wakati huo huo ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani  nchini DRC, MONUSCO umeshajipanga ili kuwezesha watoa huduma kukabiliana na changamoto ya usalama wakati wa harakati dhidi ya Ebola.

Maafias wa afya wanaokabiliana na Ebola

Tayari Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC David Gressly ametembelea Beni, ambako amepongeza serikali kwa hatua za haraka ilizochukua kutangaza kuwepo kwa ugonjwa huo.

Mangina, mji ulioko eneo la Beni jimbo la Kivu Kaskazini, ndio eneo ambako kumeripotiwa visa vya Ebola, katika mlipuko huu wa 10 wa ugonjwa huo nchini DRC.

Serikali ya DRC ilitangaza juzi mlipuko wa Ebola jimboni Kivu Kaskazini, ikiwa ni siku chache tu baada ya mlipuko huo kutangazwa kumalizika huko jimboni Equateur.

 

Tags