Aug 06, 2018 01:21 UTC
  • WHO: Nchi jirani ya DRC zichukue hatua kuzuia kuenea Ebola

Shirika la Afya Duniani WHO limesema, hali mpya ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC inazilazimisha nchi za jirani kuchukua hatua za tahadhari ili kuzuia ungojwa huo hatari kuenea.

Aidha WHO imesema kukabiliana na mlupuko mpya wa Ebola nchini DRC si kazi rahisi.

Mlipuko mpya wa Ebola uliripotiwa DRC Agosti 1 na umetokea ikiwa ni wiki moja tu baada ya WHO itangaze kutokomeza mlipuko wa awali. WHO imesema mripuko huu mpya uliotokea katika jimbo la Kivu Kaskazini hauna uhusiano na mripuko  wa ugonjwa huo uliotokomezwa kwenye jimbo la Ikweta.

Wizara ya Afya ya DRC imesema katika taarifa yake rasmi kwamba, maambukizi mapya ya ugonjwa hatari wa Ebola yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 33, mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi mkuu wa WHO, Peter Salama, zoezi la kupambana na kuumaliza ugonjwa huo uliotokea tena halitakuwa rahisi katika jimbo la Kivu Kaskazini ambalo ni makazi ya watu zaidi ya milioni 1 waliyojipatia hifadhi baada ya kuyakimbia makazi yao kutokana na vita vya kikabila katika mkoa wa Ituri.

Mwili wa mtu aliyefariki baada ya kuugua Ebola ukiwa umebebwa na wafanyakazi wa afya waliovalia mavazi maalumu

Hatari nyingine kubwa kwa mujibu wa WHO, ni kuhusu raia wa DRC wanaokimbia vita na kuvuka mpaka na kuingia kwenye nchi jirani, huku wakiwa wameambukizwa ugonjwa wa Ebola, hivyo shughuli za upimaji na uchunguzi wa kiafya zinafanywa katika sehemu zote za mpakani.

Wakuu wa sekta za afya za nchi jirani za Rwanda, Tanzania na Uganda wamewasihi wananchi kuwa watulivu na kuchukua tahadhari za kujikinga.

Katika hatua nyingine, Shirika la kudhibiti na Kuzuia Maradhi Barani Africa (Africa CDC) limeeleza kuwa, kuna umuhimu wa kuwekwa mkakati imara na ulioratibiwa vizuri ili kukabiliana na ugonjwa wa Ebola uliotokea tena wiki hii huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Tags