Aug 18, 2018 07:26 UTC
  • Athari za Ebola kwa watoto DRC ni zaidi ya kuugua –UNICEF

Watoto wanawakilisha idadi kubwa isiyo ya kawaida ya waathirika wa mlipuko wa Ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, limesema shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.

Katika taarifa ya shirika hilo, hadi sasa watoto wawili wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Hali kadhalika vituo vya kutibu wagonjwa wa Ebola katika miji ya Beni na Mangani kwenye jimbo la Kivu Kaskazini vinawapa matibabu watoto sita ambao wameambukizwa au wanashukiwa kuwa na Ebola.

UNICEF imeorodhesha watoto 53 ambao sasa ni mayatima baada ya wazazi wao kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Dkt. Gianfranco Rotigliano, anasema kuwa watoto ambao wameathiriwa na mlipuko wa Ebola wanahitaji  sio tu huduma maalum bali pia kutunzwa.

Ameongeza kuwa wanawake kimsingi ndio walezi wa kwanza wa  watoto, kwa hivyo ikiwa wameambukizwa ugonjwa huo kuna hatari kubwa ya kuambukiza watoto na familia zao. Shirika hilo likiwa na wadau wake limetoa mafunzo kwa washauri nasaha 88 ambao watasaidia kuwafariji watoto katika vituo mbalimbali na wale watoto ambao wameshatibiwa na kutoka vituoni lakini huenda wakasumbuliwa na unyanyapaa.

Dkt. Rotigliano ameongeza kuwa athari za ugonjwa huo kwa watoto sio tu kwa wale walioambukizwa au wanaoshukiwa kuwa waliambikizwa.

Watu 42 wanaripotiwa kufariki dunia kwa maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu maradhi hayo yalipoibuka tena mashariki mwa nchi hiyo mwezi huu. Huu ni mlipuiko wa 10 wa Ebola nchini DRC tokea ugonjwa huo uripotiwe kwa mara ya kwanza mwaka 1976.

 

Tags