Aug 22, 2018 07:39 UTC
  • Tanzania yakabiliwa na hatari kubwa ya mlipuko wa homa ya Ebola

Waziri wa afya wa Tanzania Bibi Ummy Mwalimu amesema, Tanzania inakabiliwa na hatari kubwa ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, ambao umesababisha vifo vya watu 50 kati ya wagonjwa 91 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Bi. Mwalimu amesema, kwa mujibu wa takwimu mpya za shirika la afya duniani WHO, mlipuko mpya wa homa ya Ebola nchini DRC umetokea kwenye maeneo yaliyo karibu na Tanzania, ikiwemo Kivu Kaskazini na Ituri.

Bibi Mwalimu amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, hadi sasa hakuna maambukizi ya virusi vya Ebola nchini Tanzania, lakini ni lazima Tanzania ichukue hatua ili kuhakikisha virusi vya Ebola havileti athari mbaya kwa Tanzania kama ilivyo DRC.

Shirika la Afya Duniani WHO limesema, hali mpya ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC inazilazimisha nchi za jirani kuchukua hatua za tahadhari ili kuzuia ungojwa huo hatari kuenea. Aidha WHO imesema kukabiliana na mlupuko mpya wa Ebola nchini DRC si kazi rahisi.

Waziri wa afya wa Tanzania Bibi Ummy Mwalimu

Mlipuko mpya wa Ebola uliripotiwa DRC Agosti 1 na umetokea ikiwa ni wiki moja tu baada ya WHO itangaze kutokomeza mlipuko wa awali. WHO imesema mripuko huu mpya uliotokea katika jimbo la Kivu Kaskazini hauna uhusiano na mripuko  wa ugonjwa huo uliotokomezwa kwenye jimbo la Ikweta.

Watu 50 wanaripotiwa kufariki dunia kwa maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu maradhi hayo yalipoibuka tena mashariki mwa nchi hiyo mwezi huu. Huu ni mlipuko wa 10 wa Ebola nchini DRC tokea ugonjwa huo uripotiwe kwa mara ya kwanza mwaka 1976.

 

Tags