Aug 25, 2018 02:21 UTC
  • WHO: Mlipuko wa Ebola DRC umeshadhibitiwa lakini hatari bado ipo

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeshadhibitiwa, lakini kuna uwezekano wa kutokea kesi mpya, kutokana na mazingira magumu yanayosababishwa na hali mbaya ya usalama na baadhi ya maeneo kutofikika.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa idara ya dharura ya WHO Dr. Peter Salama amesema, mpaka kufikia juzi (Jumatano), idadi ya maambukizi haikuzidi 100, huku kesi 103 zikithibitishwa pamoja na vifo vya watu 63. Amesema mlipuko wa sasa umezikumba wilaya sita mkoani Kivu Kaskazini na maeneo ya mkoa wa Ituri.

Dr. Salama amesema, wafanyakazi 14 wa afya wamethibitishwa ama kushukiwa kuwa na maambukizi ya Ebola, ikiwemo kifo cha mfanyakazi mmoja, hivyo kufanya kazi ya shirika hilo kwa sasa kuwa ni kuhakikisha ulinzi kwa wafanyakazi wake wa afya, ikiwemo kuwapatia chanjo na kuwapa elimu ya kujikinga na maambukizi.

Mlipuko mpya wa Ebola uliripotiwa DRC Agosti 1 na ulitokea ikiwa ni wiki moja tu baada ya WHO itangaze kutokomeza mlipuko wa awali. WHO imesema mlipuko huu mpya uliotokea katika jimbo la Kivu Kaskazini hauna uhusiano na mlipuko  wa ugonjwa huo uliotokomezwa kwenye jimbo la Ikweta.

Huu ni mlipuko wa 10 wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tokea ugonjwa huo uripotiwe kwa mara ya kwanza mwaka 1976.

Tags