Al Nahdha yapinga mpango wa Rais wa Tunisia kuhusu mirathi
Baraza la Ushauri la Harakati ya al Nahdha ncini Tunisia limetangaza kuwa linashikamana na mfumo wa mirathi ulioainishwa katika mafundisho ya Qur'ani tukufu na Suna za Mtume Muhammad (saw).
Taarifa hiyo ya Baraza Kuu la chama cha Nahdha nchini Tunisia imetolewa wiki mbili baada ya Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo kutangaza azma yake ya kuwasilisha muswada bungeni wa kufanyia mabadiliko sheria za mirathi za Kiislamu.
Baraza Kuu la Ushauri la Harakati ya al Nahdha limesema kuwa, muswada wa usawa baina ya mwanamke na mwanaume katika mirathi unapingana na sheria za Kiislamu na unazusha wasiwasi wa kutetereshwa misingi ya familia na maisha ya kijamii nchini Tunisia.
Taarifa ya baraza hilo imesisitiza udharura wa kuimarishwa zaidi haki na nafasi ya mwanamke katika sheria za Tunisia na kutekelezwa haki na uadilifu bila ya kwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu.
Chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha al Nahdha ndicho kinachoongoza kwa kuwa na viti vingi katika Bunge la Tunisia kikifuatiwa na chama cha Nidaa Tunis cha Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo.
Maelfu ya raia wa Tunisia walifanya maandamano makubwa wakipinga mapendekezo ya Rais wa nchi hiyo kuhusu mfumo wa mirathi na suala la kutambuliwa rasmi ubaradhuli na maingiliano ya kingono baina ya watu wenye jinsia moja.