UN: Hali ya raia CAR inatia wasiwasi
Ofisi ya huduma za misada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeripoti kuwa hali ya wakazi wa mji wa Alindao huko kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mbaya sana kutokana na mapigano yanayoendelea baina ya makundi ya waasi katika eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa na OCHA imesema kuwa, mapigano yanayoendelea katika mji wa Alindao na kandokando yake yamewalazimisha raia zaidi ya elfu 37 kukimbia katika kambi za wakimbizi. OCHA imesema kuwa, mji wa Alindao kwa sasa unadhibitiwa na makundi ya waasi na kwamba maafisa wa serikali katika eneo hilo wanashindwa kushughulikia matatizo ya wakimbizi hao.
Taarifa hiyo imesema kuwa mgao wa chakula kwa wakimbizi hao unatosha tu kwa kipindi cha siku 15.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.
Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na kundi la Seleka.