Keita aapa kurejesha amani nchini Mali
Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa Mali ameahidi kurejesha amani na utulivu katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Ibrahim Keita amesema hayo mjini Bamako katika sherehe za kula kiapo cha kuongoza nchi hiyo kwa kipindi cha pili na kukemea wale wanaobeza thamani za uhuru na uvumilivu wa wananchi. Amesema kuwa, hakuna jambo linaloweza kuvunja azma na mshikamano wa Wamali kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kurejesha amani na utulivu.
Hata hivyo ripoti zinasema kuwa, kiongozi huyo wa Mali anakabiliwa na kibarua kikubwa na changamoto nyingi katika awamu ya pili ya uongozi wake hususan katika upande wa masuala ya kiuchumi na usalama wa taifa. Hali ya uchumi wa Mali inaripotiwa kuwa mbaya na imewafanya Wamali wengi waishi chini ya mstari wa umaskini. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema: "Raia milioni tano na laki mbili wa Mali wanahitaji himaya na misaada ya kibinadamu."
Vilevile ukosefu wa usalama na mashambulizi ya kigaidi yameongezeka huko Mali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Ibrahim Keita alishinda uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 12 Agosti kwa kupata asilimia 67 ya kura huku mpinzani wake, Soumaïla Cissé akiambulia asilimia 33 ya kura.