Sep 09, 2018 07:16 UTC
  • Serikali yadhibiti mlipuko mpya wa Ebola Kongo DR

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza habari ya kufanikiwa kudhibiti mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola nchini humo, wiki tano baada ya kuripotiwa mlipuko wa virusi hivyo hatari.

Waziri wa Afya wa Kongo DR, Dakta Oly Ilunga Kalenga amesema tokea Agosti 13 hadi sasa, hakuna kesi mpya ya ugonjwa huo iliyoripotiwa na kwa msingi huo, serikali inawahakikishia wananchi kwamba maradhi hayo hatari yamedhibitiwa kikamilifu.

Mlipuko huu mpya uliripotiwa Agosti Mosi katika mji wa Mabalako, mkoa wa Kivu Kaskazini, wiki moja tu baada ya Shirika la Afya Duniani WHO kutangaza kuwa mlipuko wa awali wa ugonjwa huo umedhibitiwa. Alkhamisi iliyopita ugonjwa huo uliripotiwa kusambaa katika mji wa Butembo unaokadiriwa kuwa na wakazi milioni moja.

Siku chache zilizopita, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza kuwa, idadi ya wahanga wa mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola nchini humo imeongezeka na kufikia watu 89 hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi.

Chanjo ya Ebola

Tangu mwaka 2014 hadi hivi sasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshakumbwa mara kadhaa na wimbi la ugonjwa hatari wa Ebola.

Katika kipindi cha baina ya mwaka 2013 hadi 2016, virusi hatari vya Ebola vimesababisha vifo vya karibu watu 11 elfu katika maeneo tofauti duniani.

Tags