Wabunge 8 wa Chama cha Nidaa Tounes wajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48031-wabunge_8_wa_chama_cha_nidaa_tounes_wajiuzulu
Wabunge wanane wa chama cha Nidaa Tounes wamejiuzulu chamani na kujiunga na mrengo mwingine wa kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2018 23:41 UTC
  • Wabunge 8 wa Chama cha Nidaa Tounes wajiuzulu

Wabunge wanane wa chama cha Nidaa Tounes wamejiuzulu chamani na kujiunga na mrengo mwingine wa kisiasa.

Wabunge hao wa chama cha Nidaa Tounes cha Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo, wamejiunga na mrengo mwingine katika Bunge la nchi hiyo kwa jina la Muungano wa Kitaifa unaomuunga mkono Waziri Mkuu wa Tunisia Youssef Chahed. Wabunge hao juzi Jumamosi walikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu. Pande mbili hizo zilijadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya kisiasa ya Tunisia na mvutano wa kisiasa uliopo katika Serikali na chama cha Nidaa Tounes ambacho kimemtaka Waziri Mkuu Youssef Chahed ajiuzulu. 

Youssef Chahed, Waziri Mkuu wa Tunisia

Chama cha Nidaa Tounes kimekosoa mazungumzo hayo na kudai kuwa Chahed ndiye aliyewataka wajiuzulu katika chama hicho na kujiunga na mrengo wa muungano wa al Watani. Mrengo wa al Watani uliasisiwa mwezi Agosti mwaka huu na wabunge 33 wa kujitegemea na wale waliojizulu kutoka vyama vingine.

Vyama vya upinzani Tunisia vimemtaka Waziri Mkuu Youssef Chahed ajiuzulu kutokana na kushtadi matatizo ya kiuchumi na maandamano ya wananchi. Hii ni katika hali ambayo Waziri Mkuu huyo wa Tunisia katika miezi ya karibuni ametekeleza baadhi ya marekebisho katika baraza lake la mawaziri akisema kuwa amedhamiria kutekeleza marakebisho zaidi ya kiuchumi.