Sadio Mane ajibu, kwa nini anaosha choo cha msikiti, Liverpool
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48047-sadio_mane_ajibu_kwa_nini_anaosha_choo_cha_msikiti_liverpool
Mchezaji nyota wa soka wa timu ya Liverpool ya Uingereza kutoka Senegal, Sadio Mane ameeleza ni kwa nini huwa anaosha choo cha Msikiti wa Rahma mjini Liverpool.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 10, 2018 14:43 UTC
  • Sadio Mane ajibu, kwa nini anaosha choo cha msikiti, Liverpool

Mchezaji nyota wa soka wa timu ya Liverpool ya Uingereza kutoka Senegal, Sadio Mane ameeleza ni kwa nini huwa anaosha choo cha Msikiti wa Rahma mjini Liverpool.

Mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza amefichua sababu hiyo baada ya kukutana na kumhoji Mane ambaye analipwa kitita za Euro laki moja kwa wiki.

Mwaandishi huyo amemuulizi Mane kwa nini anaosha choo cha msikiti licha ya kwamba analipwa kitita kikubwa cha fedha? Nyota huyo wa timu ya taifa ya soka ya Senegal na klabu ya Liverpool amejibu kwamba anafanya hivyo kudhihirisha kuwa yeye ni Muislamu anayeshikamana na mafundisho ya dini na anayejitolea kufanya lolote kwa ajili ya dini yake.

Wiki iliyopita ilisambazwa video katika mitandao ya kijamii iliyomuonesha Sadio Mane akisaidia kazi za kusafisha maeneo ya choo cha Masjidur Rahma mjini Liverpool.  

Sadio Mane

Sadio Mane mwenye umri wa miaka 26 alizaliwa katika kijiji kidogo masikini cha Bambali huko kusini mwa Senegal na baba yake mzazi alikuwa imamu wa msikiti wa kijiji hicho; hivyo nyota huyo wa Liverpool alikulia mazingira ya msikitini.

Magazeti ya Senegal yanaripoti kuwa, baada ya kusaini mkataba na klabu ya Liverpool mwaka 2016, Mane alijitolea kuujenga umpya msikiti wa kijijini alikokulia na kushi na baba yake katika kipindi cha utotoni.