Sep 14, 2018 03:20 UTC
  • Wahanga wa Ebola waongezeka DRC

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana ilitoa taarifa mpya na kusema kuwa, wahanga wa ugonjwa hatari wa Ebola wameongezeka tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti hadi hivi sasa kiasi kwamba kati ya kesi 133 zilizosajiliwa, 102 zimethibitika kuwa ni za homa ya Ebola.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya wagonjwa 92 waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola, 61 ni miongoni mwa kesi hizo 102 waliothibitika kukumbwa na ugonjwa huo.

Wimbi jipya la kuenea virusi vya homa ya Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lilianza mwezi Mei mwaka huu katika mji wa Bikoro mkoani Ikweta, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo na baadaye kuenea katika mji wa Mbandaka, katikati mwa mkoa huo na kufika hadi mashariki mwa nchi .hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshakumbwa mara tatu na wimbi la ugonjwa wa Ebola tangu mwaka 2014 hadi hivi sasa.

Katika kipindi cha baina ya mwaka 2013 hadi 2016, ugonjwa hatari wa Ebola uliua karibu watu 11 elfu katika maeneo tofauti duniani.

Tags