Sep 15, 2018 13:52 UTC
  • UNICEF yaimarisha mikakati ya kukabiliana  na Ebola DRC

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza azma mpya ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC ili kuwasaidia maelfu ya watu, wakiwemo watoto, kufuatia kuibuka upya kwa ugonjwa huo.

Serikali ya DRC imetangaza kuwa, siku ya Alhamisi watu watano walithibitika kuwa na ugonjwa wa Ebola, wakiwemo wawili kutoka mji wa kibiashara wa Butembo katika jimbo la Kivu Kaskazini, mmoja akiwa ni mfanyakazi wa idara ya afya kutoka kituo ambacho mgonjwa wa kwanza alitibiwa.

Butembo ni mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Kivu Kaskazini, ukiwa na watu takribani milioni 1, na karibu watu wanne wamethibitika kuwa na Ebola mpaka sasa. Wagonjwa waliogundulika mapema, mmoja alifika Butembo akitokea Beni ambako ugonjwa wa Ebola ulikithiri na mwingine akitokea jimbo la Ituri na ugonjwa wake ukigunduliwa baada ya vipimo kufanyika katika kituo cha Butembo.

Hivyo UNICEF imesema inaongeza juhudi za kukabiliana na Ebola kwa kupeleka kundi la wataalam 11 mjini Butembo ili kufanya mawasiliano na jamii, kutoa elimu, kusaidia maendeleo ya kiafya na kijamii, kudhibiti usafi na kukinga vijidudu vya maradhi na kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa wa Ebola.

Kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani WHO, mpaka kufikia siku ya Jumatano, jumla ya wagonjwa wa Ebola nchini DRC imefikia 137, wakiwemo 106 waliothibitika na 31 wanaodhaniwa kuwa na ugonjwa huo. Aidha hadi sasa watu 92 wamefariki kutokana na Ebola tokea Agosti Mosi wakati mlipuko mpya wa ugonjwa huo uliporipotiwa DRC.

Tags