Essebsi: Uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa nchini Tunisia
Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia amekiri kuwa hali ni nzito hivi sasa nchini humo lakini pamoja na hayo amesisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa mwaka 2019.
Televisheni ya al Mayadeen imemnukuu rais huyo wa Tunisia akisema hayo jana na kuongeza kuwa, uchaguzi wa rais wa nchi hiyo utafanyika kama ulivyopangwa mwaka 2019 na hautowahishwa wala kuakhirishwa.
Amesema, hadi hivi sasa hajaamua iwapo atashiriki katika uchaguzi huo au la na wakati huo huo amesema kuwa kuna haja ya kufanyiwa mabadiliko Katiba ili kutatua mizozo ya kisiasa iliyopo Tunisia hivi sasa.
Rais huyo wa Tunisia pia amesema, mwafaka kati ya chama chake na kile cha al Nahdha umemalizika na kusisitiza kuwa chama cha al Nahdha kimeamua kujitoa serikalini na kufuata njia yake nyingine.
Mizozo ya kisiasa imeongezeka sana nchini Tunisia katika miezi ya hivi karibuni.
Kundi moja la watu wa serikali walifanya maandamano wiki hii wakishinikiza kujiuzulu waziri mkuu wa nchi hiyo, Youssef Chahed.
Vyama vya upinzani navyo vimetaka waziri mkuu huyo ajiuzulu kutokana na kuongezeka matatizo ya kiuchumi na malalamiko ya wananchi.
Wapinzani wa Youssef Chahed wanasema kuwa serikali yake imeshindwa kutatua mgogoro wa kiuchumi hivyo hakuna njia nyingine isipokuwa kujiuzulu yeye na baraza lake zima la mwaziri.