Shirika la Marekani lakiri kuhusu kubakwa wasichana Liberia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48823-shirika_la_marekani_lakiri_kuhusu_kubakwa_wasichana_liberia
Shirika moja la kutoa misaada ya kibinadamu la Marekani limekiri kuwa wasichana wa shule inayosimamiwa na shirika hilo walibakwa na muasisi wake na kufanyiwa jinai nyingine za kingono.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2018 23:35 UTC
  • Shirika la Marekani lakiri kuhusu kubakwa wasichana Liberia

Shirika moja la kutoa misaada ya kibinadamu la Marekani limekiri kuwa wasichana wa shule inayosimamiwa na shirika hilo walibakwa na muasisi wake na kufanyiwa jinai nyingine za kingono.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake baada ya vyombo vya habari kufichua kuhusu kashfa hiyo, shirika hilo la 'More Than Me' limesema ni kweli muasisi wa taasisi hiyo isiyo ya kiserikali, Macintosh Johnson aliwanajisi mabinti waliokuwa wakisomea shuleni hapo kwa mpangilio maalumu.

Shirika hilo limesema, "Tunaomba radhi kwa wasichana wote walionajisiwa na Johnson mwaka 2014 na kabla ya hapo. Tulikufelisheni."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, uongozi wa shirika hilo ulishindwa kusoma alama za nyakati mapema ili kuzuia ubakaji huo, uliotokea katika shule inayoendeshwa na shirika hilo katika kitongoji duni cha West Point, viungani mwa mji mkuu Monrovia. 

Ramani ya Liberia

Inaarifiwa kuwa, baadhi ya mabinti walionajisiwa walikuwa na umri wa chini ya miaka 10 na yumkini waliambukizwa virusi vya HIV kutokana na ukweli mchungu kwamba, muasisi wa shirika hilo la Marekani, Macintosh Johnson alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Shirika hilo lilitumia takriban dola milioni 8 katika harakati zake kukiwemo kufungua shule zilizokusudia kuwasaidia wasichana mwaka 2013, ambapo dola laki 6 kati ya fedha hizo zilitoka moja kwa moja kutoka serikali ya Marekani.