Liberia yachunguza visa vya ubakaji katika taasisi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48918-liberia_yachunguza_visa_vya_ubakaji_katika_taasisi_ya_marekani
Serikali ya Liberia imeanzisha uchunguzi kuhusu visa vya kubakwa wasichana wa shule inayosimamiwa na shirika moja la Marekani nchini humo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Oct 20, 2018 04:30 UTC
  • Liberia yachunguza visa vya ubakaji katika taasisi ya Marekani

Serikali ya Liberia imeanzisha uchunguzi kuhusu visa vya kubakwa wasichana wa shule inayosimamiwa na shirika moja la Marekani nchini humo.

Waziri wa Jinsia, Watoto, na Ulinzi wa Kijamii wa Liberia, Williametta Saydee Tarr jana Ijumaa alisema kamati maalumu ya kuchunguza visa hivyo vya ubakaji kwenye taasisi hiyo ya Marekani imeundwa, na itawajumuisha mawaziri wa elimu, sheria, afya, vijana, na fedha.

Siku chache zilizopita, shirika hilo la 'More Than Me' (MTM) lilikiri na kusema kuwa ni kweli muasisi wa taasisi hiyo isiyo ya kiserikali, Macintosh Johnson aliwanajisi mabinti waliokuwa wakisomea shuleni hapo kwa mpangilio maalumu.

Sanjari na kuomba radhi, uongozi wa shirika hilo umekiri kuwa ulishindwa kusoma alama za nyakati ili kuzuia ubakaji huo, uliotokea katika shule inayoendeshwa na shirika hilo katika kitongoji duni cha West Point, viungani mwa mji mkuu Monrovia. 

Watetezi za haki za binadamu Liberia wanataka taasisi ya MTM ya Marekani ifungwe

Inaarifiwa kuwa, baadhi ya mabinti walionajisiwa walikuwa na umri wa chini ya miaka 10 na yumkini waliambukizwa virusi vya HIV kutokana na ukweli mchungu kwamba, muasisi wa shirika hilo la Marekani, Macintosh Johnson alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Shirika hilo la Marekani lina shule 19 zenye wanafunzi zaidi ya elfu nne, na limepokea zaidi ya dola 600,000 kutoka serikali ya Washington za kuendeleza miradi yake ya eti kuwalinda watoto wa kike nchini Liberia.