Nov 03, 2018 02:56 UTC
  • Uganda kuanza kutoa chanjo ya Ebola kwa wafanyakazi wa sekta ya afya

Uganda imetangaza kuwa Jumatatu ijayo itaanza kutoa chanjo kwa baadhi ya wafanyakazi wake wa huduma ya afya dhidi ya maradhi ya Ebola. Hatua hiyo inachukuliwa kutokana na kuongezeka wasiwasi juu ya uwezekano wa kuenea hadi Uganda homa hiyo ya kuvuja damu inayosababishwa na virusi kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo inapambana na mlipuko wa Ebola.

Nchi hiyo ya Afrika mashariki ilishawahi kukumbwa mara kadhaa na milipuko ya Ebola na homa ya Marburg. Jane Ruth Aceng, Waziri wa Afya wa Uganda ameeleza kuwa maafisa husika wa sekta ya afya watatoa chanjo 2,100 kwa ajili ya wafanyakazi wa afya wanaofanya kazi katika wilaya zilizo karibu na mpaka wa Uganda na maeneo ya Kongo yaliyoathiriwa na Ebola. 

Dr Jane Ruth Aceng, Waziri wa Afya wa Uganda 

Amesema, makumi ya maelfu ya wananchi huvuka mpaka huo kwa wiki kwa ajili ya biashara, kutembelea familia zao na shughuli nyingine.

Waziri wa Afya wa Uganda ameongeza kuwa, kutokana na harakati hizo imebainika kuwa hatari ya kuweko maambukizo baina ya watu kupitia njia hiyo ya mpakani ni ya kiwango cha juu na kwa msingi huo kuna haja ya kuwakinga wafanyakazi wa afya na chanjo hiyo ya Ebola.  

Tags