Hofu ya Katibu Mkuu wa UN baada ya mauaji CAR
Kufuatia mashambulizi ya wiki hii nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati , CAR, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anashikamana na taifa hilo na kuonya kwamba mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia wasioweza kujitetea na walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wake Stephane Dujarric inasema “Katibu Mkuu ana hofu kubwa kufuatia kuongezeka kwa machafuko katika siku za karibuni nchini CAR.”
Guterres ameyasema hayo baada ya shambulio la Alhamisi Novemba 15 kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Alindao, kilometa 300 Mashariki mwa mji mkuu Bangui. Taarifa zinasema takribani watu 42 waliuawa kwenye shambulio ambalo lilianzishwa na kundi la waasi wa Kikristo wanaojulikana kama Anti-Balaka.
Katika shambulio lingine tofauti Ijumaa kwenye kituo cha mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo , MINUSCA katika eneo la Kusini Magharibi mwa mji wa Gbambia , mlinda amani kutoka Tanzania aliuawa. Kwa mujibu wa taarifa ya Guterres shambulio hilo linakisiwa kufanywa na kundi lenye silaha la Siriri.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakiwalinda raia waliokuwa wanapata hifadhi kwenye kijiji cha Gbambia waliposhambuliwa. Mlinda amani wa Tanzania alijeruhiwa na kufariki dunia baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata.
Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na serikali ya Tanzania. Pia amesema anaendelea kushikamana na watu na serikali ya CAR.
Katibu Mkuu amekumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na raia wasioweza kujitetea yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.
Ametoa wito kwa mamlaka ya CAR kuchunguza mashambulizi hayo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa mbele ya sharia.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.
Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na kundi la Seleka. Idadi kubwa ya Waislamu wameuawa kwa umati na wengi kulazimika kuwa wakimbizi kufuatia hujuma za genge hilo la Anti-Balaka.