'Rambo' aliyeongoza mauaji ya Waislamu wa CAR akabidhiwa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49597-'rambo'_aliyeongoza_mauaji_ya_waislamu_wa_car_akabidhiwa_icc
Mbabe wa kivita aliyeongoza kundi la wanamgambo wa Kikristo katika mauaji, utesaji na kufukuzwa makwao Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amekamatwa na kukabidhiwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2018 10:48 UTC
  • 'Rambo' aliyeongoza mauaji ya Waislamu wa CAR akabidhiwa ICC

Mbabe wa kivita aliyeongoza kundi la wanamgambo wa Kikristo katika mauaji, utesaji na kufukuzwa makwao Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amekamatwa na kukabidhiwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Alfred Yekatom ambaye zama hizo alifahamika kama 'Rambo' anatuhumiwa kuliongoza kundi la kigaidi la Anti Balaka kuwaua Waislamu wa nchi hiyo kati ya mwaka 2013 na 2014. Yekatom amekamatwa na vyombo vya dola vya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kukabidhiwa ICC, ambayo ilitoa waranti dhidi yake Novemba 11.

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi wamesema mbabe huyo wa kivita aliwaagiza wapiganaji wa 3000 wa Anti Balaka kuwashambulia Waislamu, kuwaua, kuwatesa na hata kuwafukuza katika nyumba zao, kati ya Disemba 5 mwaka 2013 na Agosti mwaka 2014,

Kadhalika anatuhumiwa kuwaingiza katika jeshi lake watoto wadogo waliokuwa na umri wa chini ya miaka 15.

Wanamgambo wa Anti Balaka

Kikao cha awali cha majaji wa ICC kilisema kina sababu za msingi za kumbebesha dhima Yekatom, kwa kuwa kipindi hicho alikuwa kamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.