Kenya yawakamata wavuvi 16 wa Tanzania kwa kuingia katika maji yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49604-kenya_yawakamata_wavuvi_16_wa_tanzania_kwa_kuingia_katika_maji_yake
Polisi ya Kenya imewatia nguvuni wavuvi 16 raia wa Tanzania, kwa kuingia katika ardhi yake na kuvua samaki kinyume cha sheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2018 00:46 UTC
  • Kenya yawakamata wavuvi 16 wa Tanzania kwa kuingia katika maji yake

Polisi ya Kenya imewatia nguvuni wavuvi 16 raia wa Tanzania, kwa kuingia katika ardhi yake na kuvua samaki kinyume cha sheria.

Wavuvi hao walikamatwa jana Jumapili karibu na ufukwe wa Bamgot, kando kando ya Ziwa Victoria. Kamishna Mkuu wa Polisi kaunti ya Migori, magharibi mwa Kenya, Joseph Nthenge amesema wavuvi hao wa Tanzania wanazuilia katika kituo cha polisi cha Macalder na kwamba watapandishwa kizimbani karibuni hivi, mara tu uchunguzi utakapokamilika.

Haya yanajiri wiki chache baada ya wavuvi 36 wa Kenya kukamatwa na vyombo vya usalama vya Tanzania, kwa kuingia na kuvua katika maji ya nchi hiyo katika Ziwa Victoria kinyume cha sheria.

Ramani inayoonesha Ziwa Victoria

Huko nyuma, wavuvi wa Kenya wamewahi kukamatwa pia na vyombo vya usalama vya Uganda, wakikabiliwa na mashitaka kama hayo ya kuingia katika maji na ardhi ya nchi hiyo kinyume cha sheria. Kenya na Uganda kwa miaka mingi sasa zimekuwa zikizozania kisiwa cha Migingo, kilichoko katika Ziwa Victoria.

Ieleweke kuwa, maji ya Ziwa Victoria yako ndani ya ardhi ya nchi tatu hizo za Afrika Mashariki, yaani Kenya, Uganda na Tanzania.