Nov 25, 2018 08:10 UTC
  • Wasichana 18 watekwa nyara na watu waliojizatiti kwa silaha Niger

Wasichana wasiopungua 18 wameripotiwa kutekwa nyara na watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kusini mashariki mwa Niger.

Meya mji wa Toumour, Boukar Mani Orthe, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, wasichana hao walitekwa na watu karibu 50 waliokuwa wamejizatiti kwa silaha usiku wa kuamkia jana, katika vijiji vya Blaharde na Bague, yapata kilomita 9 nje ya mji wa Toumour, ulioko katika mkoa wa Diffa, kusini mashariki mwa nchi.

Ingawaje hakuna kundi lililotangaza kuhusika na utekaji huo kufikia sasa, lakini magenge ya kigaidi yenye mfungamano na kundi la ukufurishaji la Boko Haram yanashukiwa kutokana na faili lao jeusi la vitendo hivyo vya kikatili.

Alkhamisi iliyopita, watu wanaoaminika kuwa na mfungamano na genge la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram waliishambulia kampuni ya kuchimba visima vya maji ya Ufaransa ya Foraco kusini mashariki mwa Niger na kuua watu wanane.

Mwaka 2014, Boko Haram iliwateka nyara wasichana 276 wa Chibok nchini Nigeria

Shambulizi hilo la wanachama wa Boko Haram lilifanyika katika mji huo wa Toumour mkoani Diffa. Mkoa huo wa Diffa mara kwa mara umekuwa ukishambuliwa na magaidi wa Boko Haram ambao wana maficho yao katika nchi jirani ya Nigeria.

Miezi michache iliyopita, askari kumi wa Niger waliuawa katika hujuma ya Boko Haram katika mkoa huohuo ulioko kusini mashariki mwa nchi, karibu na mpaka na Nigeria.

Tags