Sababu za mivutano ya sasa ya kisiasa nchini Tunisia
Chama cha Nidaa Tounis kimemtuhumu Waziri Mkuu wa Tunisia kuwa anafanya jitihada za kumpindua rais wa nchi hiyo, madai ambayo yamepingwa na Waziri Mkuu na kuzusha mvutano mkubwa wa kisiasa nchini humo.
Mwezi Agosti mwaka 2016 Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia alimwamuru Youssef Chahed kuunda serikali mpya ya Tunisia. Katika kipindi cha miezi 27 iliyopita Chahed amefanya mabadiliko mara mbili katika serikali yake na mara ya mwisho ilikuwa tarehe 6 mwezi huu wa Novemba ambapo alibadilisha mawaziri 13. Hatua hiyo imepingwa na Rais Beji Caid Essebsi anayesema hakushauriwa kabla ya kuchukuliwa hatua hiyo na kwamba Waziri Mkuu amepuuza nafasi ya Rais wa nchi katika marekebisho ya baraza la mawaziri. Msemaji wa Rais wa Tunisia, Saida Garrach amesema: Essebsi haafikiani na njia zilizotumiwa na Waziri Mkuu kwa ajili ya kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri.
Hali hii imemfanya Katibu Mkuu wa chama cha Nidaa Tounis, Salim Al Riahi amtuhumu Waziri Mkuu wa Tunisia, Youssef Chahed ambaye aliteuliwa na chama hicho kuwa Waziri Mkuu kwamba, amefanya mapinduzi dhidi ya Rais Beji Caid Essebsi kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika ndani ya baraza la mawaziri bila ya kushauriana na rais wa nchi.
Swali muhimu linalojitokeza hapa ni kuwa, ni nini sababu ya mivutano ya sasa nchini Tunisia?
Sababu kuu ya mivutano hiyo ni hitilafu za ndani ya chama cha Nidaa Tounis. Youssef Chahed ambaye ni mwanachama wa chama hicho na mkwe wa Rais Beji Caid Essebsi amekuwa akimtuhumu kiongozi huyo na mwanaye, Hafez Caid Essebsi ambaye ndiye kiongozi wa chama tawala kuwa wanakwamisha utendaji wa serikali yake. Chahed anasema kuwa, Hafez Caid Essebsi anafanya jitihada za kumuondoa katika nafasi ya Waziri Mkuu na kuchukua nafasi hiyo. Essebsi na mwanaye wamekanusha madai hayo. Wajumbe wa chama cha Nidaa Tounis pia walikuwa tayari wametoa wito wa kusailiwa Youssef Chahed ndani ya chama hicho. Wito huo umepingwa na Youssef Chahed ambaye amesema ni mpango wa mapinduzi dhidi yake uliobuniwa na Caid Essebsi. Kwa msingi huo mwezi Septemba mwaka huu Tume ya Masuala ya Siasa ya Chama cha Nidaa Tounis ilichukua uamuzi wa kusimamisha uanachama wa Chahed kwa tuhuma za kuzusha mgawanyiko na kuanzisha mgogoro ndani ya chama hicho.
Suala jingine kuhusu mivutano ya sasa katika serikali ya Tunisia ni kwamba Youssef Chahed anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusu utendaji usiofaa wa serikali yake hususan katika sekta ya uchumi. Kwa kadiri kwamba, Alkhamisi iliyopita wafanyakazi karibu laki saba wa umma walifanya maandamano wakilalamikia hali mbaya ya uchumi na mishahara yao. Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Youssef Chahed amedai maandamano hayo yalipangwa na Caid Essebsi siku kumi baada ya Bunge la Tunisia kupiga kura ya kuwa na imani na mawaziri wapya wa serikali ya nchi hiyo.
Sababu ya tatu ya mivutano ya kisiasa nchini Tunisia ni hatua ya Youssef Chahed ya kumteuwa mfanyabiashara wa Kiyahudi, Rene Trabelsi kuwa Waziri wa Utalii wa nchi hiyo, sauala ambalo limepingwa sana ndani ya Tunisia. Baadhi ya wachambuzi wa mambo waaamini kuwa, sababu ya kuteuliwa mfanyabiashara huyo Myahudi kuwa Waziri mpya wa Utalii wa Tunisia ni sera za Chahed za kutaka kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel. Hata hivyo Waziri Mkuu wa Tunisia amejibu tuhuma hizo akisema: “Nimesikia mengi kuhusu suala la kutaka kuanzisha uhusiano na Israel lakini napenda kusisitiza kuwa, suala la kuwaunga mkono watu wa Palestina kwa ajili ya kupata haki zao halali na kuunda dola huru daima limekuwa msimamo thabiti na usiobadilika wa Tunisia.”
Kwa ufupi ni kwamba, hali ya sasa ya Tunisia haitoi bishara njema ya kumalizika salama mivutano na mgogoro unaoshuhudiwa sasa ndani ya chama tawala cha Nidaa Tounis.